Viongozi wa Kaunti ya Baringo wakiongozwa na Gavana Stanley Kiptis wamo matatani baada ya kukiuka amri zilizoletwa na serikali kupunguza kuenea virusi vya Covid-19.
Viongozi hao walihutubia umati mkubwa wa wananchi mji wa Kabarnet bila kuzingatia umbali wa kijamii.
Wakazi walijaa nje ya majengo ya bunge la kaunti wakikaidi wito wa maafisa wa afya na usalama wa umma ya kujitenga na kuzingatia umbali wa kijamii kuzuia Covid-19.
Wananchi wengi pia hawakuwa wamevalia maski na ilibidi Gavana Kiptis kuwaagiza maafisa wake kuwagawia wenyeji.
Viongozi hao na wenyeji walikusanyika wakitaka kuhamishwa kwa Kamishna wa Kaunti Henry Wafula ambaye walimshutumu kwa kuagiza kukamatwa kwa Mwakilishi wa Wadi ya Bartabwa Reuben Chepsongol, juu ya matamshi ya chuki, anayodaiwa alitamka Ijumaa.
“Kwa kweli tunajua watu wanastahili kuwa nyumbani wakati huu wa janga la corona lakini tunalazimika kukusanyika ili kudai kuondolewa kwa Wafula” Kiptis alisema.
Mnamo Jumamosi Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alitangaza kuwa nchi ya Kenya imesajili kesi 16 zaidi, na kuongeza idadi ya maambukizo kufikia 262.
Viongozi wengine ambao walikuwa katika mkutano huo ambao ulidumu kwa saa moja ni pamoja na mbunge wa Baringo Kaskazini William Cheptumo, mwenzake wa Baringo Kusini Charles Kamuren, Spika wa Bunge la Kaunti ya Baringo David Kiplagat na Naibu Gavana Jacob Chepkwony na Wakilishi wa Wadi kadhaa.